10 July 2012

Ukabila ni adui wa Maendeleo Tanzania



Na Daniel Samson

NI rahisi kwa nadharia kusema Tanzania haina ukabila lakini sio rahisi kuthibitisha kwa vitendo kuwa hakuna tatizo hilo.

Ukabila ni dhana ambayo kwa wakati huu inatajwa sana katika vyombo vya habari, wanasiasa  na hata wananchi wakawaida wameipa nafasi kubwa katika mazungumzo yao ya kila siku.

Ikiwa ukabila umepata mashiko katika harakati za maisha ya watu ni vyema suala hili kulipa nafasi ya kulijadili kwa kina kwani waswahili husema kuwa, lisemwalo lipo na kama halipo linakuja.

Kwa kutumia msemo huu tujiulize ukabila upo katika nchi yetu? Au ni suala la kufikirika lakini halina umuhimu wowote katika maendeleo.

Lakini ukabila nini? na kuna umuhimu gani wa kuzungumzia suala ambalo ni dhana ambayo inakuzwa na watu wachache kwa nia ya kukidhi matakwa yao ya kisiasa ili kujinufaisha na mfumo wa maisha ambao utawafanya watu wengine katika jamii kujiona wametengwa na kubaguliwa.

Ukabila “Tribalism” maana yake rahisi ni sisi na wao, sisi ni bora na wao hawana sehemu na sisi. Ukabila unasababishwa na ubinafsi wa watu katika kutekeleza majukumu ya maendeleo katika jamii ambayo ina watu wenye mtazamo, itikadi, dini, lugha na tamaduni tofauti.

Tofauti hizi husabisha jamii moja kujitenga na jamii nyingine hivyo kuibua matabaka ya watu ambao kila mmoja anajiona ni bora kuliko mwenzake.

Watu huunda makundi ambayo hujitenga na jamii nyingine ambazo hazina mwelekeo sawa na kundi lao. Kutokana na kuibuka kwa makundi haya husababisha tofauti kubwa ya maendeleo kati ya jamii moja na nyingine.

Kama hilo halitoshi migogoro isiyoisha baina ya pande hasimu huzuka na hivyokusababisha vita visivyoisha ambavyo huzolotesha juhudi za kujiletea maendeleo.

Ukabila hujitokeza ndani ya nchi ambayo huwa na vikundi na makabila ambayo yanazungumza lugha tofauti na kusambaa katika maeneo mbalimbali. Lakini ukabila pia unaweza ukawa baina ya taifa moja na jingine ambayo kimsingi huendeleza dhana ya utaifa na kujitenga na taifa lingine katika nyanja zote za maisha.

Chanzo cha migogoro na matatizo mengi Afrika leo ni ukabila
(usisi na uwao) ambayo yamesababisha vita visivyoisha, njaa, umaskini na uharibifu wa rasilimali muhimu kwa maendeleo.

Ukabila umeanza kurudi nchini baada ya kudhibitiwa kwa
mda mrefu lakini sasa dalili zinajidhihirisha katika maeneo kadhaa, kutokana na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi ambayo jamii inapitia.

Tanzania ni nchi yenye  makabila zaidi ya mia moja na ishirini ambayo huzungumza lugha tofauti lakini inaunganishwa na lugha kuu ya kiswahili ambayo hutumika katika mawasiliano hasa katika shughuli za maendeleo.

Pamoja na kuwepo na tofauti za makabila bado wananchi wake
wanashirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ikilinganishwa na nchi nyingine kama Nigeria ambayo imegawanyika katika makabila makuu manne ya Hausa, Igbo, Yaruba na Fulani ambayo yana nguvu na uhasimu mkubwa ambao umewafanya  wagawanyike na kuunda serikali za majimbo zinazotofautiana..

Kabla ya ukoloni kuingia Afrika watu waliishi maisha ya ujima ambayo watu hukaa pamoja na kumiliki njia za uzalishaji ambazo mgawanyo wa utajiri ulikuwa sawa kwa
makundi yote bila matabaka.

Wakoloni walipokuja Afrika na kuanza kututawala walitumia njia ya kutugawa katika makundi  ili umoja wetu usiwepo tena na kuwa rahisi kwao kutumia rasilimali zilizopo bila kipingamizi.

Hapa ndipo ukabila ukachipuka na maeneo mengi ya Afrika yakabaki nyuma katika harakati za maendeleo kwa sababu umoja haukuwepo tena.

Mwaka wa 1961 Tanzania ikipata uhuru kutoka katika koloni
la Muingereza, kazi iliyokuwepo ni kuyaunganisha makabila  yaliyokuwa na utamaduni na lugha tofauti. Mwalimu Julius Nyerere, mwasisi wa taifa hili akatumia utashi na uongozi bora kuyaunganisha makabila yote na kukemea vikali ukabila kwa sababu wakati huo nchi ilikuwa inahitaji umoja na mshikamano wa kulijenga taifa kiuchumi na kisiasa.

Lugha ya kiswahili ilitumika kuwaunganisha watu na kuondoa
tofauti zilizokuwepo, na watu walitahadharishwa madhara ya ukabila na hilo likafanikiwa japokuwa kulikuwa na tofauti ndogo ambazo hata leo zipo.

Sababu iliyofanya ukabila usiwe na nguvu  miaka  iliyopita   ilikuwa mgawanyo mzuri wa utajili wa nchi. Kutokana na msingi huu uliojengwa nchi yetu ikawa ni mfano wa kuigwa kwa nchi nyingine ambazo zina migogoro isiyoisha ambayo chanzo chake ni ukabila.

Dhana ya ukabila imeanza kuibuka kwa kusikika katika mazungumzo ya watu na viongozi wa nchi wakisema umoja tulionao tuutumie vizuri na tusiruhusu tofauti zetu zitugawe na kuturudisha katika zama za ukoloni ambazo watu waligawanywa kwa itikadi na mtazamo.

Lakini tujiulize kwa nini suala hili linaibuka wakati huu? Na watu wameona nini mpaka wanalipigia kelele? Haya ni maswali ya msingi ya kujiuliza na tunahitaji kuyapatia majibu ndipo tutafute suluhisho la tatizo lililo mbele yetu.

Kuna mambo yanayofanyika leo katika jamii yanawatenga watu wa jamii fulani na kujiona hawathaminiwi na hivyo kuhitaji kujitenga ili kuendeleza rasilimali zilizopo katika maeneo husika.

Wengine katika mikutano ya kisisasa wanapiga kelele za serikali za majimbo lakini suala la kijitenga lina changamoto zake tusifanye maamuzi bila kufanya
utafiti wa kina  kabla ya  kupanda mbegu  ambayo inaweza kutugharimu miaka ijayo.

Zanzibar ikiwa ni sehemu moja ya muungano tayari malalamiko
yanasikika  kuwa hawatendewi haki katika mgawanyo wa rasilimali.

Vimeibuka vikundi vya watu  wanaopiga kelele za kujitenga lakini malalamiko mengi yanatokana na kero za Muungano na watu wengine visiwani wanafikia hatua ya kusema wabara warudi kwao.

Dhana ya utengano ni dalili mbaya kwa mstakabali wa taifa  ambalo jamii zote zimeishi kwa amani mda mrefu lakini kuna haja ya kulitazama hili kwa makini kwa sababu ukabila unajitokeza kwa sura mbalimbali.

Kuna mambo ambayo yanatendeka na watu wachache yanaashiria muendelezo wa ukabila katika nchi yetu. Mfano maeneo ya kazi na katika ofisi za umma, sio ajabu ukawakuta watu wa kabila moja wameshika nyadhifa muhimu za uongozi na kuchukuliwa kama eneo hilo ni la kabila fulani. Sababu hii inaweza isiwe na nguvu ya kisheria kwa kuwa kila ofisi ina sheria za kuajiri wafanyakazi wenye sifa bila kuangalia huyu
anaotoka kabila au dini gani kwa sababu misingi ya serikali
haijajengwa katika  kabila lolote.

Ikiwa ofisi ya umma ina wafanyakazi wengi wa kabila fulani na
wana sifa muhimu za kufanya kazi hakuna tatizo, wasiwasi unakuja pale undugu kutawala katika ajira yaani bila kuwa na uhusiano wa karibu na mtu fulani katika ofisi  huwezi kupata nafasi  na hivyo wakati mwingine watu wenye sifa hawajiriwi.

Kiswahili ni lugha ya mawasiliano katika kuendesha shughuli za serikali, lakini maofisini watu huzungumza lugha za makabila yao kitu ambacho kinaleta picha mbaya kwa watu ambao hawajui lugha husika huku wengine wakijiuliza kinachotokea.

Undugu ambao umesababisha shughuli za serikali katika idara mbalimbali kutokufanyika kwa kiwango kinachotakiwa kwa kuwa taratibu za kuajili watu hazizingatiwi na wafanyakazi kuwaweka watu ambao wataendeleza maslai yao.

Ukabila pia unajitokeza kwa wasomi wa vyuo vikuu ambao wanategemewa na jamii kupinga dhana hii ambayo huendeleza ubaguzi na tofauti zisizo na msingi halali. Vyuo kama taasisi zina watu wa kada mbalimbali ambao huunda vikundi vya kijamii ili kuwakutanisha kupanga mipango ya
maendeleo.

Wasiwasi unakuja pale watu wa kabila fulani kuunda kikundi
na kuendesha mambo yanahusu kabila fulani pekee. Makundi haya hayajumuishi makabila na watu wote
wanaotoka katika wilaya husika. Katika mbao zao za matangazo katika vyuo utaona wameandika “wanachama wa kabila fulani mnatakiwa kukutana mahali kujadili maendeleo ya jimbo lenu”

Kwa nini wasikutane wote kutoa mchango katika kuleta maendeleo ya jimbo husika.

Tabia hii inapanda mbegu ya umimi  ambayo sio nzuri kwa wasomi ambao wanategemewa na serikali kuleta maendeleo ya jamii yote bila kujali itikadi na makabila yaliyopo kwa sababu wote sisi ni watanzania na tunaunganishwa kwa lugha moja ya Kiswahili.

Tabia hii ikiachwa iendelee hujitokeza mahali pa kazi ambapo watumishi  kuajili watu wa kwao hata kama hawana sifa za kutimiza majukumu, kwa sababu ni vigumu kwa tabia
kujitokeza ghafla lakini huanza mbali hasa katika mfumo wa utendaji wa taasisi mbalimbali za umma.

Ukabila ambao unajitokeza wakati huu unakuja kwa sula ya udini na watu kuanza kujitambulisha kwa dini zao badala ya utaifa. Udini ambao umeanza kujitokeza na watu kupigania maslai ya dini zao na kuacha kutafakari mstakabali wa nchi na jinsi ya kujikwamua katika umaskini.

Serikali haina dini wala kabila  watanzania tupinge fikra finyu za watu wachache ambao wanakuza udini  na ukabila kwa sababu bado dini zetu zinatuanganisha katika mambo mengi ya maendeleo na hivyo hakuna haja ya kutengana  kwa  tofauti zetu.

Tuwakatae watu wachache kutumia silaha ya ukabila na udini kwa maslahi ya kisiasa ili kudhohofisha juhudi za mabadiliko katika jamii na mshikamano uliopo Tanzania. Jamii hasa viongozi wa nchi kutatua malalamiko ya watu na kuhakikisha watu wanapata mahitaji yao bila upendeleo.

Utengano ni udhaifu bali umoja ni nguvu, watanzania tutatue tofauti zetu na kuungana kwa pamoja kuleta maendeleo katika taifa letu.

No comments:

Post a Comment