15 March 2013

Muhubiri mbaroni kwa uchochezi



Na Suleiman Abeid, Shinyanga

MUHUBIRI wa dini ya Kikristo, mkazi wa Kigogo, Dar es Salaam, Damian Ndhimbo (35), juzi alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu, akituhumiwa kusambaza nyaraka mbalimbali zinazodaiwa kuwa za uchochezi.

Nyaraka hizo zinadaiwa kupinga kitendo cha Waislamu kuendelea kuchinja nyama kwa ajili ya kitoweo.

Mbele ya Hakimu Thomson Mtani, Mwendesha Mashtaka wa mahakama hiyo, Kiduadi Karinga, alidai mshtakiwa alikamatwa
Machi 8 mwaka huu, saa 12 jioni, akiwa ndani ya Kanisa la
Katoliki Parokia ya Nyalikungu akitoa mahubiri ambayo
yangeweza kusababisha uchochezi.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mbali ya kutoa lugha ya uchochezi mshtakiwa pia alikamatwa na CD za video na nyaraka za kupinga suala la uchinjaji kwa Waislamu.

Karinga alisema vitu hivyo vingeweza kusababisha uvunjifu wa
amani miongoni mwa waumini wa dhehebu la Kikristo na Kiislamu.

Hata hivyo, mshtakiwa alikana mashtaka hayo na kesi yake kuahirishwa hadi Machi 22 mwaka huu itakapotajwa tena
na yuko nje kwa dhamana.

3 comments:

  1. Nadhani polisi na waendesha mashitaka wanapaswa kuwa makini na kazi zao kwani kukurupa kushitaki watu kwawezi kuwa sehemu ya uchochezi wenyewe. Je kuna sheria gani inayosema mkristo hauruhusiwi kuchinja au ni mwislamu pekee ndiyo anaruhusiwa kuchinja? kukurupuka kushitaki kunaweza kuwachochea wakristu kujiuliza kulikoni serikali inasimamia na kutetea dini moja (waisilam) pekee na kuwafanya wengine kufanyakazi hiyo ni kosa la jinai? Busara zaidi inahitajika katika kutatua mgongano huo wa kimaslahi kwani tatizo la misingi ni kuwa uchinjaji sasa ni ajira na hakuna sheria inayombagua mtu kwa kupata ajira kwa kigezo cha dini yake au imani yake. Chondechonde polisi na waendesha mashitaka msikimbilie na kukurupuka kushitaki watu bila utafiti, mtu huyo hana kesi ya kujibu na kesi hiyo inapaswa kufutwa kabla haijaibua chuki kwa wakristo!!

    ReplyDelete
  2. Polisi watafute chanzo na watumie busara zaidi kwa vile sioni wanatoa suluhu ipi katika hili kwani hili ni suala la wenye imani na wasio na imani kuzungumza pamoja wakaelewana kama ilivyokuwa zamani.Sasa hivi wakristo wanasubiri ni kifungu gani cha sheria ya uchinjaji ya wapi wataitumia.Mbona kuna cd nyingi tu zinazohimiza vurugu na hawazikamati?

    ReplyDelete
  3. Jambo la msingi zaidi katika hili Polisi lazima watumie busara zaidi kuliko kukimbilia mahakamani kwa kigezo cha uchochezi wa mhubiri huyo.Napenda kuelewa zaidi ni huyo mhubiri TU aliye mchochezi au kuna wengine? Hizi CD zinazouzwa kwenye library mbalimbali nazo JE Mawaidha yaliyorekodiwa humo na yenyewe tusemeje? Nashauri busara itumike zaidi kuliko kukimbilia mahakamani. Inatubidi tuwe makini sana na maamuzi yetu tusije kuwa sehemu ya uchochezi huo.

    ReplyDelete