- MCT,CHADEMA,NCCR, TAASISI ZATOA TAMKO
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto
Kabwe (CHADEMA), ametoa taarifa kwa katibu wa Bunge kwa mujibu wa kanuni za
Bunge kuelezea kusudio lake la kuwasilisha mswada binafsi wa marekebisho sheria
ya magazeti ili ifutwe kabisa, anaripoti Anneth Kagenda na Darlin Said.
Taarifa aliyoitoa Dar
es Salaam jana kwenye vyombo vya habari, ilisema lengo la kushawishi kufutwa
kwa sheria hiyo ya mwaka 1976 ni kwa sababu inakinzana na Katiba ya Nchi juu ya
haki za raia kupata habari.Alisema mswada huo
atauwasilisha Ijumaa ili uchapwe katika gazeti la Serikali uweze kuingia kwenye
shughuli za Bunge ambazo zitaanza Oktoba 15 mwaka huu, ngazi ya kamati.
Mkurugenzi wa Habari
na Uenezi wa CHADEMA, Bw. John Mnyika, amemshauri Bw. Kabwe auwasilishe mswada
huo kama wa haraka kwani ukienda kwa taratibu
za kawaida, kuna vikwazo vya kikanuni, kiserikali na kibunge.Alisema vikwazo hivyo
vitatumika kuukwamisha kwa kuzingatia wakati suala hilo limelenga kuyanusuru magazeti
yasiendelee kufungiwa hivyo hatua za haraka zinahitajika.
Aliongeza kuwa, kwa
mujibu wa kanuni za bunge, mswada wa mbunge binafsi ukipelekwa, kawaida
serikali ndiyo yenye kazi ya kuuchapa katika gazeti la serikali kabla ya kwenda
Kamati za Bunge na bungeni hivyo unaweza kukwamishwa.
Katika hatua nyingine, Baraza la Habari nchini (MCT) limelaani uamuzi wa serikali
kuyafungia magazeti hayo yakidaiwa kuchapisha habari za uchochezi na kujenga
chuki ili kuushawishi umma ukose imani na vyombo vya serikali.
Taarifa iliyotolewa
kwa vyombo vya habari jana, ilisema hatua zilizochukuliwa na serikali si za
kidemokrasia na zimeirudisha nchi miongo 10 nyuma katika jitihada zake za
kujenga jamii ya kidemokrasia ambayo inaheshimu uhuru wa kujieleza na uhuru wa
vyombo vya habari.
“Uhuru wa kujieleza
ni muhimu zaidi kuliko haki zote, nchi inayodai kufuata kanuni za kidemokrasia
na maadili ya haki za kibinadamu kama Tanzania inapaswa kulinda haki hii
ya msingi.“Serikali inapaswa
kutafuta njia nyingine za kurekebisha matukio ambayo wanadhani ni uwakilishaji
mbaya wa kazi zake unaofanywa na vyombo vya habari pamoja na kufanya
mazungumzo,” alisema.
Baraza hilo limewataka wadau wa
vyombo vya habari na umma kwa ujumla kuunga mkono juhudi zake za kukazania
kufutwa kwa sheria mbaya zinazokandamiza uhuru wa kujieleza, vyombo vya habari pamoja
na upatikanaji habari.
Wakati huo huo, wanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu na wadau
mbalimbali, wametoa tamko la kupinga kufungiwa kwa magazeti ya Mwananchi na
Mtanzania na kuiomba Serikali iyafungulie mara moja.
Tamko hilo lilisomwa na Mratibu
wa Mtandao huo (THRD-Coalition), Onesmo Olengurumwa, kwa niaba ya wenzake mbele
ya waandishi wa habari na viongozi mbalimbali wa mitandao hiyo zaidi ya 50.
Alisema ni vyema
Serikali ikatumia njia shirikishi kama
mahakama na Baraza la Habari nchini (MCT) kupeleka malalamiko yake badala ya
kuvifungia vyombo hivyo.“Serikali izifute na
kuzifanyia marekebisho sheria zote kandamizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya
habari, kufungiwa kwa vyombo hivi kunaleta hofu kwenye jamii,” alisema.
Katika hatua nyingine,
Mkuu wa Idara na Taasisi za Dola na Vyombo vya Uwakilishi wa Chama cha
NCCR-Mageuzi Bw. Faustine Sungura, alisema wamesikitishwa na kitendo cha
Serikali kuyafungia magazeti hayo wakati wananchi wanahitaji taarifa hasa
kipindi hiki cha katiba.
Alisema Serikali imeamua kuyafungia magazeti hayo bila kuwatangazia
wananchi nani mlalamikaji wa mwenendo mbaya wa magazeti hayo kama
ilivyodai serikali.
No comments:
Post a Comment