10 October 2013

WADAU WA HABARI WAMFUNGIA DKT. MUKANGARA, MWAMBENE


Na Rachel Balama
  Wadau wa habari hapa nchini wameazimia kusitisha kuandika , kutangaza na kupiga picha shughuli zozote zitakazowahusisha au kuratibiwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fennella Mukangara na Msemaji wa Serikali Assah Mwambene hadi hapo itakapotangazwa vinginevyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, wadau hao walitoa tamko hilo jijini Dar es Salaam jana wakati walipokutana kujadili mwendelezo wa Serikali wa kufungia vyombo vya habari.
Wadau hao walisema kuwa, adhabu hiyo inaanza mara moja kuanzia jana na kuongeza kwamba wataendelea kupinga Sheria ya Magazeti ya mwaka 1979 kwa kupigia kelele kufutwa kwa sheria hiyo.
Walisema, pia wataongeza nguvu ya kisheria mahakamani kwenye kesi iliyofunguliwa na kampuni ya Hali halisi Publishers Ltd, mwaka 2009 inayopinga sheria hiyo ambapo waliwaomba wananchi wawaelewe kwa kuchukua hatua hiyo.
  Pia wadau hao walidai wamesikitishwa na hatua ya Serikali ya kutosikiliza kilio cha wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri, waandishi, taasisi za vyombo vya habari, wasambazaji wa magazeti na watu wengine wa kawaida juu ya kuyaondolea adhabu magazeti matatu ya Mwanahalisi, Mtanzania na Mwananchi yaliyofungiwa na Serikali.
"Aidha, wadau wamesikitishwa na hatua ya Serikali ya kupuuza kilio chao cha kuomba kusitishwa kwa Sheria Kandamizi ya Magazeti ya mwaka 1976 na kudhoofisha mchakato wa kuibadilisha sheria hiyo iliyotajwa na Tume ya Jaji Francis Nyalali mwaka 1992 kuwa ipo kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," ilieleza taarifa hiyo.
  Uamuzi huo ulifikiwa na wadau hao kutoka Chama cha Wamiliki wa vyombo vya Habari (MOAT), Jukwaa la Wahariri (TEF), MISA Tan, Baraza la Habari Tanzania (MCT), Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Dar City Press Club (DCPC) na Tanzania Human Rights Defenders (THRDC)..

No comments:

Post a Comment