27 November 2013

ZITTO KUJIBU MASHTAKA 11



  •  BARUA ZATOLEWA RASMI,WAPEWA SIKU 14

  • BAADA YA MAJIBU,KUJIELEZA KAMATI KUU

  • LISSU ADAI UTETEZI WAO ULIPOTOSHA UKWELI

 Na Goodluck Hongo
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Zitto Kabwe pamoja na wenzake, wameandaliwa mashtaka 11 kwa madai ya kuandaa mapinduzi ya siri dhidi ya uongozi wa chama hicho kinyume cha katiba.

Bw. Kabwe na wenzake ambao ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Dkt. Kitila Mkumbo na Bw. Samson Mwigamba, aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA jijini Arusha, jana walikabidhiwa barua rasmi ili wajieleze ndani ya siku 14.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, Bw. John Mnyika, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho.
Bw. Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Dar es Salaam, alisema chama hicho kimeandaa mashtaka hayo baada ya Sekretarieti ya CHADEMA kupitia maamuzi ya Kamati Kuu yaliyowavua nyadhifa za uongozi watuhumiwa hao.
 "Watuhumiwa hawa watatakiwa kujieleza kwa maandishi ndani ya siku 14, baadaye watajieleza mbele ya Kamati Kuu ambayo itatoa maamuzi ya hatua za kuchukua," alisema Bw. Mnyika.
Alisema mashtaka hayo yametokana na waraka wa siri ambao ulikamatwa na kutolewa mbele ya Kamati Kuu unaowakashifu viongozi wakuu wa chama hicho.
"Wote watatakiwa kujieleza kwa nini wasifukuzwe ndani ya chama chetu kwa makosa waliyofanya... Kamati Kuu ya chama ndicho chombo chenye maamuzi ya kuwaondoa viongozi au wanachama wanaokiuka Katiba.
"Waraka uliochapishwa katika baadhi ya vyombo vya habari (si Majira) na mitandao ya kijamii unaodaiwa kuwaponza Bw. Kabwe na wenzake si wenyewe ni batili," alisema.
Aliongeza kuwa, maamuzi yaliyofanywa na Kamati Kuu yalizingatia kanuni, sheria na taratibu za chama kwa kufuata katiba, hivyo Bw. Kabwe na wenzake hawakufukuzwa kwa sababu walizozitoa kwenye vyombo vya habari bali kwa kuandika waraka wa kimapinduzi.
Msimamo wa CHADEMA
Bw. Mnyika alisema, chama hicho hakipo tayari kuwavumilia viongozi na wanachama wote ambao watakuwa kikwazo kwa chama hicho kufikia malengo yake bila kujali cheo alichonacho.
"Wanatafuta huruma kwa wananchi kutokana na makosa ambayo wameyafanya hasa la kuandaa waraka wa siri, wao wenyewe walikiri kuhusika nao lakini wanapotosha ukweli," alisema.
Alisema Sekretarieti hiyo imepokea na kutoa mapendekezo mbalimbali ya utekelezaji wa mikakati waliyojipangia ambayo ni Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) na "CHADEMA ni msingi".
Akizungumzia uchomaji wa bendera za chama, ofisi, fulana na kuondoa mabango ya CHADEMA, baada ya Bw. Kabwe na wenzake kuvuliwa nyadhifa za uongozi, Bw. Mnyika alisema chama kimezisikia taarifa hizo.
"Uchunguzi wa awali unaonesha kilichotokea ni kiini macho tu si wanachama wa chama chetu waliofanya hivyo, viongozi wa maeneo husika wanaendelea na vikao, usalama upo," alisema.
Tundu Lissu azungumza
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Bw. Tundu Lissu, alisema watuhumiwa walifanya mkutano na vyombo vya habari kwa lengo la kupotosha ukweli wa mambo juu ya mazingira halisi ya kuvuliwa nyadhifa zao.
"Hawakuondolewa katika nyadhifa zao kwa sababu ya kuuza majimbo yetu ya uchaguzi mwaka 2010, si posho, wala uwepo wake kama Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), aliyeibua hoja ya kukaguliwa kwa hesabu za vyama vya siasa.
"Amevuliwa nyadhifa hizo na wenzake kwa sababu ya kuandaa mapinduzi ndani ya chama kwa kukiuka maadili," alisema.
Akizungumzia madai ya kugawanyika au kupasuka kwa chama hicho kama Bw. Kabwe atafukuzwa uanacham, Bw. Lissu alisema kwa nyaraka alizoziona, Kabwe alikuwepo katika kikao cha Kamati Kuu kilichomfukuza aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho mwaka 2004, Dkt. Amaan Kabourou.
"Ka bwe p i a a l i k uwe p o kwenye kikao cha Kamati Kuu kilichomfukuza aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hiki, marehemu Chacha Wangwe mwaka 2007; hivyo hata kikao kama hicho ndicho kilichowavua vyeo yeye na wenzie hivyo Kamati Kuu isilaumiwe," alisema.
Bw. Lissu alisema, madai ya Bw. Kabwe kudai alijitoa katika utiaji saini katika masuala ya fedha ndani ya chama hicho kwanza hakuwahi kuwa mtiaji saini ili kuidhinisha fedha, hivyo anashangaa kulizungumzia hilo wakati hakuwahi kuwa mtiaji saini.
"Chama kimepasuka mara nyingi tangu enzi ya Bw. Kabwe kuingia kwenye Kamati ya Jaji Bomani, Chacha Wangwe, ugaidi wa Rwakatare hata sakata la mabomu lakini tuliibuka upya, hadi sasa chama kinaendelea na mapambano yake," alisema.
Alipoulizwa na waandishi kama viongozi hao wakiamua kuondoka, chama kimejipangaje, alisema si vizuri kuwahukumu Bw. Kabwe na wenzake kwa sababu bado hawajaanza kujitetea, lakini kugombea uongozi ndani ya chama si uhaini wala dhambi.
Alibainisha kuwa, sh. milioni 100 zilizotolewa na mfanyabiashara maarufu nchini, Bw. Mustafa Sabodo, hesabu za matumizi yake zipo wazi na zilipelekwa kwenye hesabu za chama hicho ili zikaguliwe na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Aliongeza kuwa, licha ya vyama vya siasa kuwa tayari kukaguliwa, CAG alishindwa kukagua hesabu hizo kwa sababu ya ukosefu wa fedha, hivyo alivitaka vyama husika kuwalipa wakaguzi ambao wangefanya ukaguzi huo jambo ambalo walilipinga.
"Tuna ushahidi wote kuhusu suala hili, hata Msajili mpya wa Vyama vya Siasa, aliandika barua kwa CAG kuhusu kupinga vyama kuwalipa wakaguzi wa hesabu  kwani huo si utarabu wa Serikali, lakini tunamshangaa Kabwe kuzungumzia suala hili wakati analijua vizuri," alisema Bw. Lissu




No comments:

Post a Comment